Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO
wanakutana leo mjini Brussels kutathmini mkakati wa pamoja, baada
ya kile wanachokiita "mwaka wa uchokozi" nchini Ukraine na
Mashariki ya Kati na pia kujadili kumalizika kwa kampeni yao ya
kijeshi nchini Afghanistan. Mawaziri hao pia watajadili juhudi za NATO
kuwahakikishia usalama wao wanachama wake wa mataifa ya
mashariki mwa Ulaya, mukiwemo doria ya ndege za kijeshi, meli na
wanajeshi wa ardhini. Mkuu mpya wa NATO, Jens Stoltenberg,
amesema mkutano huu unakuja wakati Urusi ikiwa imejiingiza Ukraine
na kitisho cha kundi lijiitalo Dola la Kiislamu kikiendelea nchini Iraq na
Syria, na kwamba mwaka 2014 umekuwa mwaka wa uchokozi,
migogoro na mizozo. Mwezi Septemba mwaka huu, viongozi wa
mataifa 28 wanachama wa NATO, walikubaliana kuunda kikosi cha
dharura kukabiliana na changamoto zisizotegemewa, wakisema sasa
wanakabiliwa na kitisho kipya kwa usalama wa eneo lao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni