Kenyatta amtaka Nkurunziza kuahirisha uchaguzi
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amemtaka Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza kuahirisha uchaguzi mkuu nchini mwake unaotarajiwa mwezi ujao baada ya jaribio la mapinduzi dhidi ya utawala wa Nkurunziza kushindwa wiki iliyopita. Msemaji wa Rais wa Kenya Manoah Esipisu amesema viongozi hao wawili wa nchi za jumuiya ya Afrika Mashariki walizungumza hapo jana kwa njia ya simu. Espisu amesema viongozi wengine wa nchi za kanda hiyo ya Afrika Mashariki wana mtizamo sawa na Kenyatta. Viongozi hao wanataka uchaguzi huo kuahirishwa kwa misingi ya kuwa hakuna mazingira mazuri ya kuendesha uchaguzi huo wa tarehe 26 mwezi Juni. Wakati huo huo, Marekani imesaidia kuwaondoa raia wake na wa nchi nyingine za kigeni kutoka Burundi hapo jana baada ya nchi hiyo kukumbwa na ghasia kufuatia maandamano ya wiki kadhaa na jaribio la mapinduzi wiki iliyopita dhidi ya Rais Nkurunziza. Rais Nkurunziza alionekana kwa mara ya kwanza hadharani hapo jana tangu jaribio hilo la mapinduzi kufeli.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni